KATAMBI AAMUA KUPAMBANA NA CHADEMA ' KAMA WANASHAMBULIA MTU KWA UONGO..NITASEMA UKWELI WAZI WAZI.....


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi amesema tuhuma zinazoelekezwa kwake kwamba amenunuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hazina ukweli.

Katambi ambaye jana alitangaza kujiunga na CCM ametoa kauli hiyo kipindi ambacho kumekuwa na tuhuma zinazoelekezwa kwake ikiwamo ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwamba ameshawishiwa na akakubali.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 22, Katambi amesema hakuna mtu yoyote anayeweza kumnunua huku akisema Chadema kimepoteza dira hivyo wenye uelewa wataondoka.

“Nimesikia mengi, nitafanya mkutano na waandishi wa habari, nilidhani wangejitathimini katika ukweli ili kusaidia vijana, chama na taifa lakini kama wanaamua kushambulia mtu kwa uongo bila ushahidi, nitasema ukweli waziwazi,” amesema Katambi

Kuhusu tuhuma za rushwa, Katambi amesema ‘’Katambi hanunuliki wala hana bei naishi katika Principle…kwa wenye akili wangejua dira imepotea watafute upya masafa.”

Awali leo asubuhi, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akizungumza na Mwananchi kuhusu kuondoka kwa Katambi amesema;

"Badala ya nguvu na fedha kuzielekeza kujenga viwanda wao nguvu wamezielekeza kushawishi viongozi wetu, wamewashwishi wengi na Katambi ni miongoni ingawa wengine wamekataa."

Na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527