JESHI LA ZIMBABWE : TUNACHUKUA HATUA KUWALENGA WAHALIFU....RAIS MUGABE YUKO SALAMA

Jeshi la Zimbabwe limesoma taarifa kwenye kituo cha runinga cha serikali ZBC, likisema kuwa linachukua hatua ya kuwalenga wahalifu.

Hata hivyo limesema kuwa hayo sio mapinduzi ya kijeshi na Rais Mugabe yuko salama.

Milio mikubwa ya risasi ilisikika katika maeneo ya kaskazini mwa mji mkuu Harare mapema leo.

Taarifa hiyo ya jeshi ilikuja saa kadhaa baada ya jeshi kudhibiti kituo cha ZBC.

Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa sare za jeshi alisema kuwa jeshi linataka kukabiliana na watu ambao wanatenda uhalifu unaoleta madhara ya kijamii na kiuchumi nchini Zimbabwe.

"Wakati tutakapomalzia wajibu wetu, tunatarajia kuwa hali itarudi kuwa sawa."

Taarifa hiyo ilisema kuwa Mugabe 93, na familia yake wako salama.Wanajeshi wakiwa na silaha nzito wameoneakana wakirandaranda mjini Harare

Haijulikani ni nani anaongoza hatua hiyo ya kijeshi.

Magari ya wanajeshi waliojihami kwa silaha yameonekana maeneo ya mjini Harare.

Hali hiyo ya wasi wasi wa lolote kuweza kutokea, imeanza hapo jana jioni, ambapo wanajeshi wakiwa na silaha walionekana wakijipanga katika maeneo kadhaa pamoja na kuzingira ofisi za shirika la utangazaji la Zimbabwe ZBC.

Hata hivyo taarifa zinasema kuwa wafanyakazi wa shirika hilo la utangazaji ZBC, waliambiwa na wanajeshi hao kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi na kwamba uwepo wa vikosi hivyo ni kwa lengo la kulinda eneo hilo.

Milipuko mizito imeendelea kusikika pia.Mkuu wa jeshi la Zimbabwe Constantino Chiwenga alitahadharisha uwezekano wa jeshi kuchukua nchi

Chama tawala nchini Zimbabwe kimemtuhumu mkuu wa majeshi Constantino Chiwenga, kwa hatua yake ya madai kuwa jeshi lipo tayari kuingilia mzozo huo wa kisiasa kwa lengo la kulinda wapigania uhuru wa taifa hilo.

Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na Rais Robert Mugabe kutokana na hali ya sasa nchini mwake.

Marekani imesema kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya Zimbabwe na kutoa rai pande zote kutatua mzozo huo kwa njia ya amani.Grace Mugabe anaonekana kukaribia kukirithi kiti cha mumewe

Naye Balozi wa Marekani nchini Zimbabwe kupitia ukurasa wake wa Tiwtter amesema kuwa leo watasitisha shughuli za kiofisi ubalozini hapo kutokana na halisi ya sasa mjini Harare.

Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika Kusini Isack Moyo ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa serikali ipo imara katika jambo hilo na kuzuia uwezekano wowote wa kufanyika kwa mapinduzi.
Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527