RAIS MAGUFULI ATAKA TAASISI ZA AGA KHAN KUPUNGUZA GHARAMA ZA MATIBABU


Rais John Magufuli akiagana na kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia duniani, Prince Karim Al-Hussayni Aga Khan baada ya kufanya naye mazungumzo alipomtembelea Ikulu, Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).

***
RAIS John Magufuli ametoa mwito kwa Taasisi za Aga Khan kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi ili waweze kumudu, hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.

Rais Magufuli alisema hayo jana alipokutana Ikulu Dar es Salaam na Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia Duniani, Karim Aga Khan ambapo alimshukuru kwa taasisi zake kutoa huduma za kijamii hapa nchini.

Pia Rais Magufuli alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Aga Khan na amemuomba kiongozi huyo kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake, ikiwa ni pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.

Akizungumza na Rais, Aga Khan alisema Jumuiya ya Ismailia imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua hospitali ya Aga Khan iliyopo Dar es Salaam na kujenga chuo kikuu kikubwa katika Afrika Mashariki mkoani Arusha.

Aga Khan alisema kuwa upanuzi wa hospitali ya Aga Khan, utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia vitanda 172, utaimarisha matibabu ya moyo, kansa na utaongeza ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.

Kuhusu chuo kikuu kitakachojengwa Arusha, Aga Khan alisema Jumuiya hiyo imedhamiria kujenga chuo kikuu kikubwa ambacho kitafundisha viongozi si tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali pia Afrika nzima ili waweze kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya Afrika.

Kwa upande wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Aga Khan, alisema kuwa yeye haamini kuwa yeye ni kipaumbele kwa vyombo vya habari kujikita katika masuala ya siasa. Badala yake, alisema anaamini kuwa vyombo vya habari vina wajibu mpana zaidi wa kujikita katika masuala ya maendeleo hususani katika nchini zinazoendelea, na kwamba Aga Khan ipo katika mchakato wa kujikita katika wajibu huo kwa kuwa na waandishi wa habari na wachambuzi mahiri.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Maseneta wa Baraza la Seneti la Marekani, ambao ni wajumbe wa kamati ya mazingira inayoshughulikia hifadhi ya taifa, wanyamapori na misitu ya Marekani, ambao wamekuwepo hapa nchini kwa siku tatu kwa lengo la kutembelea hifadhi ya taifa ya Ngorongoro.

Maseneta hao ni James Inhofe, Mike Enzi, David Perdue, Luther Strange, Tim Scott na John Thune. Baada ya mazungumzo hayo, Seneta James Inhofe na Seneta Mike Enzi walimshukuru Rais Magufuli kwa kukutana nao na kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza nchini.

Walikiri kuwa Tanzania inazo rasilimali nyingi ambazo ni fursa muhimu ya kukuza uchumi. Mazungumzo kati ya maseneta hao na Rais Magufuli, yalihudhuriwa pia na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inmi Patterson.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments