RAIS MAGUFULI AMLILIA ASKOFU CASTORY MSEMWA ALIYEFARIKI DUNIA AKIWA OMAN

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi Mhashamu Castory Msemwa, kilichotokea tarehe 19 Oktoba, 2017 nchini Oman.


Mhashamu Askofu Castory Msemwa amefariki dunia Mjini Muscat akiwa safarini kuelekea nchini India kwa Matibabu.


"Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Baba Askofu Msemwa, kilichotokea huko Oman, Baba Askofu Msemwa ametoa mchango mkubwa sio tu katika kutimiza majukumu yake ya huduma za kiroho bali pia katika kuisaidia jamii kupata huduma mbalimbali anazostahili binadamu na amekuwa akitoa ushirikiano mkubwa kwa taasisi nyingine zikiwemo za Serikali katika kudumisha amani, upendo, umoja na kuwahudumia wananchi, mchango wake utakumbukwa daima" Amesema Mhe. Rais Magufuli.


Mhe. Rais Magufuli amemuomba Rais wa TEC Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kumfikishia pole nyingi kwa Maaskofu wote wa TEC, Mapadre, Makatekista na waumini wote wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa msiba huu mkubwa uliotokea na amesema anaungana nao katika kipindi cha majonzi na maombi kwa Marehemu.


"Raha ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Askofu Castory Msemwa apumzike kwa amani, Amina" Amemalizia Mhe. Rais Magufuli.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527