WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wamesema baada ya hukumu ya
Bunge sasa wanasubiri neno la Rais.
Viongozi hao waliyasema hayo jana, ikiwa ni siku chache tangu Bunge kupendekeza mamlaka za uteuzi ziwavue madaraka.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), ilionyesha viongozi hao walifanya makosa kadhaa na
kusababisha uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti ya
Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Viongozi wengine ambao mamlaka zao za uteuzi zilitakiwa kuwavua
nyadhifa zao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka ambaye aliingiziwa Sh bilioni 1.6, Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge, Sh bilioni 1.6 na Waziri wa zamani wa Nishati
na Madini, William Ngeleja Sh milioni 40.
Profesa Muhongo alisema: “Sina maoni,
sasa wewe unataka kujua nini… kwani wewe umeonaje na ni lazima nikujibu
au unataka nikujibu porojo… sasa nakujibu kwamba kaulize Bunge kuhusu
hilo suala la Escrow na kama una maswali kuhusu mambo ya umeme nenda
Tanesco watakujibu.”
Jaji Werema: Siwezi kubishana na Bunge
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alisema hana kauli wala maoni yoyote na hawezi kubishana na Bunge.
“Siwezi kubishana na Bunge kwa sababu wenye mamlaka wamepewa kazi
kuchukua hatua, acha wafanye kazi, au unataka nisemeje tena?” alihoji
Jaji Werema.
Hatima ya Askofu Kilaini, Nzigilwa
Kanisa Katoliki nchini limesema haliwezi kuwaadhibu maaskofu wake
waliotajwa kuingiziwa fedha zilizotokana na kashfa hiyo kwa sababu
wanawajibika kwa kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Francis.
Maaskofu wa kanisa hilo waliotajwa kwenye kashfa hiyo ni Askofu
Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini aliyedaiwa kupewa Sh
milioni 80.5 na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigilwa, Sh milioni 40.4.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi jana, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la
Maaskofu wa Katoliki (TEC), Askofu Severin Niwemugizi, alisema hadi sasa
hawajataarifiwa kama kuna kosa limefanyika, hivyo hawawezi kukutana.
“Kama kungekuwa na kosa angetaarifiwa rais wa baraza… kwakuwa hakuna kosa hakuna dharura yoyote ya kusema tukutane.
“Kama kanisa hatuna sababu ya kusema tuhamaki tuwaadhibu kwa sababu
askofu yuko chini ya baba mtakatifu,” alisema Askofu Niwemugizi.
Hata hivyo, alisema kama vyombo vya dola vikifanya uchunguzi na
kubaini kuna makosa ya kinidhamu au kijinai, hapo ndipo wanaweza
kuchukua hatua.
“’Unless’ uchunguzi ukifanywa wakasema kuna makosa ya kijinai na kinidhamu taratibu nyingine zinaweza zikachukuliwa.
“Jambo hili linazungumzwa kisiasa zaidi na ukweli haukusemwa bungeni…
hizi ni mbio za urais, sasa wanataka kuwaingiza na wengine ambao
hawahusiki,” alisema.
Kuhusu Benki ya Biashara ya Mkombozi ambayo ilihusika kupitisha fedha
hizo, Askofu Niwemugizi alisema ilifuata taratibu zinazotakiwa ndiyo
maana walienda Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) ili kujiridhisha.
“Benki inafanya biashara, na mteja anapoleta fedha wanafuata taratibu
zinazotakiwa, benki nyingine ziliona wivu kwa kukosa hizo fedha na ndio
wanaochochea,” alisema.
CAG mpya kuipitia Ripoti ya IPTL
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Juma Asaad,
amesema kazi yake ya kwanza ni kuipitia tena ripoti ya ofisi yake juu ya
Akaunti ya Tegeta Escrow iliyojadiliwa bungeni hivi karibuni.
Profesa Asaad aliyasema hayo baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
“Nikianza kazi nitaipitia ripoti ya IPTL ambayo ilizua mjadala mkubwa
katika Bunge hivi karibuni kwa sababu sijui kilichoandikwa, lakini
nikiisoma na kutumia uzoefu wangu nitaweza kujua kinachoendelea,”
alisema Asaad.
Alisema pia atafanya kazi kwa uadilifu na uaminifu ili kuhakikisha
anatenda haki kwa kila atakayehusishwa na ripoti ili Serikali iweze
kuchukua uamuzi.
“Siwezi kumuonea mtu, bali nitafanya kazi kwa uadilifu ili
kuhakikisha kuwa natenda haki kwa kila mmoja, kwa sababu nina uzoefu wa
mambo hayo, hivyo basi nitahakikisha haki inatendeka.
“Hii ni dhamana kubwa kwangu niliyopewa na rais, siwezi kumwangusha,
hivyo basi nitahakikisha natimiza majukumu yangu kwa mujibu wa sheria
ili ripoti zote ziwe na kiwango,” alisema.
Christopher Ole Sendeka
Siku chache baada ya Bunge kupitisha maazimio nane kuhusu kashfa ya
Escrow, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), ameibuka na
kusema baadhi ya wabunge walipokea rushwa ili kupoza mjadala bungeni.
Alisema rushwa ilivyokuwa inagawiwa kama njugu mjini Dodoma
ilisababisha baadhi ya wabunge kutetea hoja za kuwalinda watuhumiwa
jambo ambalo halikuwa sawa.
Akizungumza nakwa njia ya simu, Sendeka ambaye
anafahamika kwa misimamo yake, alisema baadhi ya wabunge ambao
waliipinga ripoti ya CAG na ile ya PAC hawakuwa na nia njema.
Baadhi ya wabunge waliokuwa vinara wa kutetea watuhumiwa na kupinga
ripoti hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi, Asumpta
Mshama (Nkenge), Livingstone Lusinde (Mtera) na Richard Ndassa (Sumve)
wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa
Ghasia.
Ole Sendeka alisema pamoja na kwamba hana ushahidi wa kimahakama,
lakini kulikuwa na dalili za wazi za kuwapo vitendo vya rushwa kutolewa
kwa baadhi ya wabunge.
“Siwezi kuwa na ushahidi wa kimahakama, lakini kulikuwa na dalili za
wazi za rushwa kutolewa nje nje bila aibu na ndiyo maana ulishuhudia
namna wengi walivyokuwa hawataki kuona ukweli ukisemwa na wakati
mwingine kuwatetea mafisadi huku wakiwatupia kashfa wengine,” alisema
Sendeka.
Alisema ni jambo lililo dhahiri kwamba kulikuwa na rushwa kutokana na baadhi ya wabunge kubadili misimamo yao ya awali.
“Hata wale ambao kawaida yao walikuwa na misimamo katika mambo ya
msingi na taifa kwa ujumla, walibadilika ghafla jambo lililotushangaza
na hilo lilituaminisha kwamba kulikuwa na rushwa ilitolewa kwa sababu
haiwezekani mtu kutetea vitu ambavyo viko wazi,” alisema.
Taarifa hii imeandaliwa na Nora Damian, Patricia Kimelemeta na Elizabeth Hombo
Habari za Mapenzi,Simulizi za Mapenzi na Visa vya Mapenzi utazipata Kwa Kubofya Hapa
Habari za Mapenzi,Simulizi za Mapenzi na Visa vya Mapenzi utazipata Kwa Kubofya Hapa
Social Plugin