Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MZIMU WA PESA ZA ESCROW WAHARIBU HALI YA HEWA HUKO GEITA

 

KUTOKANA na kashifa kubwa sana inayowakabili baadhi ya Mawaziri na Wabunge wa chama cha mapinduzi (CCM) ya kuchota zaidi ya Bilioni 300  kwenye akaunti ya Tegeta Escrow baadhi ya wananchi Mkoani Geita wametakiwa kutowapa dhamana ya uongozi wenyeviti wa serikali za mitaa wanaotokana na CCM Bali wachague wenyeviti wa CHADEMA ili kuweza kuwadhibiti wezi hao kuanzia chini.

Kauli hiyo imetolewa jana na mjumbe wa Mkutano mkuu Taifa Chadema,Tecla Johaness kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni wa kuwanadi wagombea wawili kupitia Chadema wa mtaa wa Elimu,Ezekiel Matesa na mgombea wa mtaa wa Uwanja, Joseph Msoma.

 Mkutano huo uliofanyika katika kiwanja cha shule ya msingi Nyankumbu ulihudhuriwa na mamia ya wananchi ukiwa ni mwendelezo wa mikutano inayofanywa na Chadema katika Jimbo la Geita kunadi wagombea wa uenyekiti wa mitaa,vitongoji na vijiji.

Tecla alisema endapo wananchi wa Tanzania wakiwachagua wenyeviti wengi wa CHADEMA kuliko  wa CCM  wataweza kudhibiti wizi  unaondelea hata kwenye baadhi ya Halmshauri  kwani viongozi wa CHADEMA ni watetezi wa wanyonge kama wanavyoona Bungeni.

“Jamani nawaomba wananchi wangu wote wachagueni wagombea hawa waliojitokeza kupitia CHADEMA, najua wote wana uwezo wa kutosha wa kuweza kutatua shida zenu na kupambana na wizi unaoendelea katika taifa letu” alisema Tecla.

Katika hatua nyingine Tecla alimtaka Rais wa Jamhuri ya Tanzani Jakaya Mrisho Kikwete kuwafukuza kazi mawaziri wawili  ambao ni Anna Tibaijuka na Sospeter Muhongo kutokana na kuiba pesa nyingi  kwenye akaunti ya  Tegeta Escrow ambazo ni kodi za wananchi.

Kwa upande wake Ezekiel Matesa anayegombea mtaa wa Elimu katika kata mpya ya Nyankumbu alisema kuwa, endapo atapewa dhamana ya kuongoza mtaa huo atahakikisha uwanja wa shule ya msingi Nyankumbu uliouzwa na CCM unarudishwa mara moja kutokana na wanafunzi hao wa Nyankumbu kukosa pa kuchezea.

Kwa upande wa tatizo la umeme ambalo limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa mtaa huo japo upo katikati ya mji wa Geita, huku aliyekuwa mwenyekiti wa mtaa huo kupitia CCM  akizidi kutoa huduma hiyo kwa gharama kubwa kwa kutumia Jenereta  alisema wananchi wameshindwa kumudu gharama hivyo kuahidi kulifanyia kazi.
Naye mgombea wa mtaa wa Uwanja,Joseph Msoma alisema kuwa atapambana na tatizo la maji na upimaji wa viwanja katika mtaa wake.

Pia alidai kuwa kuna tatizo la ukosefu wa umeme maana umeishia mtaa jirani wa Mbugani.

Uchaguzi wa serikali za mitaa utafanyika 14 Desemba 2014 huku Jimbo la Geita likionekana Chadema kuikaba vikali chama cha mapinduzi katika uchaguzi huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com