CCM YAPITA BILA KUPINGWA VITONGOJI 211 JIMBO LA SOLWA SHINYANGA,MBUNGE ASEMA WANAOJIPANGA KUMNG'OA WANAOTA NDOTO ZA MCHANA

 Mbunge  wa jimbo  la  Solwa  Ahmed  Salum 

Vitongoji  211 katika jimbo la Solwa halmashauri   ya wilaya  ya  Shinyanga  vimepita bila kupingwa  kati 856 vilivyopo, baada ya vyama vingine vya upinzani kushindwa  kusimamisha   wagombea hivyo nafasi  kuchukuliwa  na  chama kimoja na kushindwa   kuleta  ushindani kwa  wanaogombea  nafasi  hiyo.
Hayo  yalibainishwa juzi  na  katibu wa  chama  cha  mapinduzi CCM  wilaya ya  Shinyanga  Magreth   Cosmas  wakati  akitoa  taarifa kwa  katibu wa mkoa wa chama hicho  Maganga  Sengerema, kwenye  uzinduzi wa  kampeni  za  uchaguzi  wa  serikali  za  mitaa katika  kata  ya Iselamagazi ,huku  akiweka  wazi  kuwa hiyo ni  dalili  ya kupata ushindi wa  kishindo.
Katibu  huyo  alisema mbali  na  vitongoji  hivyo  pia  vijiji 13  kati  ya  126   kwenye  jimbo  hilo vimepita bila  kuwa na upinzani .
Katika hatua nyingine  aliwataka  vijana  kuacha  kutumiwa  kama  daraja  na  baadhi ya  vyama  vya siasa kuongoza maandamano   na  kusababisha  vurugu  ambazo  zinaweza  kufanya   waishie  kufungwa  na kupoteza  mwelekeo wa maisha.
Akizungumza kwenye  uzinduzi wa kampeni  mbunge  wa jimbo  la  Solwa  Ahmed  Salum  aliweka wazi  kuwa atagombea  tena katika  uchaguzi  mkuu  ujao na  kwamba wanaopita  na kusema watamuangusha  wanaota  ndoto ya mchana
Mbunge huyo aliongeza kuwa kamwe  hawezi  kuachia nafasi   hiyo kwa  kuwa amelitoa  mbali  jimbo mpaka   ahakikishe wananchi  wanapata huduma  zote  muhimu.
Alisema wataendelea  kuboresha  huduma  zote muhimu  ikiwamo  afya,elimu, maji  ,umeme  na  miundombinu  ya  barabara ili  kuwarahisishia  upatikanaji  wa  huduma ,ambapo  aliwaomba wananchi  kuchagua viongozi  wa mitaa,vitongoji na wajumbe wote  wa  CCM  hatua itakayorahisisha  utendaji kazi   wenye tija kwa  kuwa wataongea  lugha moja.
Kwa upande  wake  katibu  wa CCM  mkoa wa   Shinyanga  Maganga  Sengerema  alisisitiza  juu ya  kuendelea  kuienzi amani,upendo  na mshikamano  uliopo   kwa  watanzania na kujiepusha  na  vitendo  viovu  vitakavyoweza kuvuruga,kwani  kuirudisha  ni  gharama  kubwa  iwapo  wataichezea na kuwaasa  wananchi  kuwa  makini  na wanasiasa   wanaotoa  kauli za  uchochezi.
Uchaguzi  wa  serikali  za  mitaa unatarajiwa  kufanyika nchi nzima  Desemba  14  mwaka  huu  ambao  utachagua  wenyeviti  wa  mtaa,vitongoji na  wajumbe, katika mkoa  wa Shinyanga tayari  CCM  imepita  bila  kupingwa katika vitongoji   456 kati  ya 2761  na  vijiji  70  kati   ya  511 vilivyopo.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

BOFYA HAPA KUSOMA HABARI ZA MAPENZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527