Na Mwandishi wetu, Dar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Disemba 09, 2025, Tanzania ikiadhimisha miaka 64 ya uhuru wa Tanzania bara, ametangaza kuwasamehe wafungwa 1,036, wafungwa 22 kati yao wakiachiliwa huru na wengine 1,014 wakipunguziwa adhabu zao.
Kulingana na taarifa iliyosainiwa na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mhe. George Simbachawene, Ikulu imeeleza kuwa ni matarajio ya serikali kuwa wafungwa walioachiwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa Taifa na kujiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.
Miongoni mwa waliosamehewa ni wafungwa wagonjwa wenye magonjwa ya kudumu au sugu ambao wapo katika hatua za mwisho pamoja na wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi- Vyote vikitakiwa kuthibitishwa na jopo la waganga wa Wilaya na Mikoa.
Aidha wengine walionufaika na msamaha huo ni wafungwa wa kike walioingia na ujauzito gerezani au wenye watoto wanaonyonya au wasionyonya waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na kuendelea pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili wasio na uwezo wa kufanya kazi.
Aidha wamesamehewa pia wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kuwekwa kizuizini (under president's pleasure) ambao wamekaa gerezani kuanzia miaka kumi au zaidi

Social Plugin