Tanzania Bloggers Network (TBN) imetoa salamu maalum kwa Watanzania katika maadhimisho ya miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania, ikisisitiza umuhimu wa kutafakari historia ya Taifa, mafanikio yaliyopatikana na wajibu wa kizazi cha sasa katika kuendeleza misingi ya amani, umoja na maendeleo.Akitoa salamu hizo, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe amesema kuwa siku ya Uhuru si tukio la kawaida, bali ni wakati muhimu wa kuenzi dhamira ya waasisi wa Taifa waliopigania uhuru ili Watanzania wajitegemee na kuendelea kujenga nchi yenye misingi imara.
Tujenge Taifa, Tuache Kulibomoa
Mwenyekiti huyo amesema TBN kama chombo cha habari za kidijitali kinaona umuhimu wa kuendeleza gurudumu la maendeleo kupitia utulivu, maridhiano na mshikamano.
Amebainisha kuwa mafanikio mengi ya Taifa yamejengwa juu ya msingi wa amani, na bila misingi hiyo hakuna Taifa linaloweza kupiga hatua.
Katika kusisitiza umuhimu wa kutunza amani, Msimbe alinukuu pia kauli ya Rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyesema:“Amani si kitu cha asili, tunahitaji kuilinda na kuitunza kila siku. Bila amani, hakuna maendeleo ya kweli.”
Amesema kuruhusu vurugu, uchochezi na mifarakano kunadhoofisha juhudi za waasisi wa Taifa katika kupambana na maadui watatu—ujinga, umaskini na maradhi—na kwamba Watanzania wanapaswa kuepuka kutumiwa kama chombo cha kuharibu misingi ya Taifa.
Msimbe amekumbusha umuhimu wa kuheshimu falsafa ya uongozi wa kila kizazi, akinukuu maneno ya Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliyewahi kueleza: “Kila utawala na zama zake. Kila kiongozi na mchango wake katika ujenzi wa Taifa hili.”
Amesema kwamba chini ya uongozi wa sasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Taifa linajikita katika dhana ya 4R — Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding — ambayo inalenga kuimarisha maridhiano, mageuzi na ustahimilivu kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wote.
Katika salamu hizo, TBN imewataka Watanzania kutumia uhuru wa maoni na mitandao ya kijamii kwa busara kwa ajili ya kuimarisha umoja na sio kubomoa Taifa. Msimbe alisema ni wajibu wa kila mwananchi “kutunza amani, kufanya kazi kwa bidii na kuacha kutumika kama chombo cha kuharibu nchi.”
TBN imetoa salamu za heri kwa Watanzania wote katika maadhimisho ya Miaka 64 ya Uhuru, ikisisitiza kauli mbiu yake:“Tanzania Kwanza, Kazi na Utu — Tusonge Mbele.”
Social Plugin