KATIBU MKUU WA CCM AMLIMA BARUA WAZIRI MKUU


 Ni siku 20 tu zimepita tangu Dk Bashiru Ally ateuliwe kuwa katibu mkuu wa CCM, lakini ameshafanya mambo makubwa; amemuandikia barua tatu Waziri Mkuu.


Dk Bashiru anamtaka kiongozi huyo wa shughuli za Serikali bungeni ashughulikie mambo matatu ili chama hicho kikongwe kiendelee kuaminika ili kichaguliwe na wananchi kuendelea kuongoza nchi.


Wakati Dk Bashiru akisema amemlima barua Waziri Mkuu, mtangulizi wake katika nafasi hiyo, Abdulrahman Kinana amewaaga wabunge wa chama hicho, akiacha wosia ulioibua hisia tofauti miongoni mwao.


Wawili hao walisema hayo juzi usiku jijini Dodoma katika hafla iliyoandaliwa na wabunge wa CCM mahsusi kwa ajili ya kumuaga Kinana, ambaye amejijengea heshima kama kiongozi aliyekirejeshea uhai chama hicho katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


Wakati Kinana alitumia majukwaa ya kisiasa kuwachongea viongozi wabovu kwa wananchi, Dk Bashiru amesema atajikita zaidi katika utendaji na kupiga marufuku viongozi wa kariba hiyo kupanda majukwaani.


Na hotuba zao za juzi zilionyesha wazi tofauti ya utendaji wa wawili hao.


Akizungumza katika hafla hiyo, Dk Bashiru aliyekabidhiwa ofisi na Kinana Mei 31, alisema CCM haiwezi kuaminika “kama chama cha umma, chama cha wanyonge kama hatuwezi kutatua matatizo ya ardhi yanayowakumba wananchi hasa maeneo ya hifadhi”.


“Tunataka chama kiongoze Serikali na tunaposema chama ni wabunge na kamati yenu hii ambayo ni ya kikatiba na hii ni Serikali ya CCM, iwe karibu na wananchi,” alisema Dk Bashiru.


“Waziri Mkuu, tangu nimeingia nimekupiga barua tatu. Moja ya mgogoro wa ardhi wa Chanika (Dar es Salaam), ya ma -DC (wakuu wa wilaya) na RC (wakuu wa mikoa) kutohudhuria vikao vya kamati za siasa, na nyingine ya mipango ya maendeleo kuandikwa kwa Kiingereza wakati inakwenda kwa wakulima na wavuvi.


“Na ujipange zinaweza kufika 100 au 1,000. Tunataka chama kinachokwenda kutatatua matatizo ya wananchi.”


Mgogoro huo wa ardhi wa Chanika ambao umedumu kwa miaka 20 unahusu mgogoro wa mpaka kati ya wakazi wa Chanika na msitu wa hifadhi wa Kazimzumbwi, wakati wakuu wa wilaya na mikoa ni wajumbe wa vikao vya CCM vya ngazi zao.


Mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliwataka wabunge wa CCM wasiwe na wasiwasi na kung’atuka kwa Kinana kwa kuwa mabadiliko ndani ya chama na Serikali hayaepukiki.


“Nimekuja tuzungumze, ili tuanze kazi pale alipoishia Abdul. Katika mabadiliko yoyote hasa ya chama kikubwa yanayofanywa na CCM, ni mabadiliko makubwa mawili,” alisema.


“Husababisha msisimko wa matarajio makubwa na upande mwingine mabadiliko huwa na tabia ya kuzaa wasiwasi na kupata wasiwasi na matarajio huhitaji ushirikiano mkubwa na hili ndilo linatokea.


“Kwa kuondoka Abdul kuna wasiwasi. Tusidanganyane. (Kinana) Ameondoka (hivyo) kuna matarajio mnayasubiri kutoka kwa Bashiru,” alisema Dk Bashiru.


“Lakini si Abdul wala Bashiru tunaoweza kuleta uwiano sawa. Kama kuna watu wamekaa tayari kumzomea Bashiru kusubiri kuona uwiano wa Abdul na Bashiru, hao si wana CCM ni mashabiki.


“Wana CCM lazima tuyadhibiti na kufika kule tunakokwenda. Hotuba kubwa ya ndugu yangu (Kinana) imetoa mwelekeo wapi tunakwenda na kazi yangu nawaahidi, nitaanzia pale alipoishia Abdul; kuongoza mapambano ya chama chetu ili wale wanaosubiri kuona tukiyumba washindwe.”


Alisema kazi ya kwanza ni uchaguzi wa serikali za mitaa, akitaka vitendo zaidi ili kushinda na hivyo kupata hamasa ya kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.




Kanuni zimepitwa na wakati


Lakini Kinana, mbali na kuwa na ujumbe huo wa kufanya jitihada kushinda uchaguzi ujao, alijielekeza katika mambo yanayotakiwa kurekebishwa ndani ya chama hicho, ikiwa ni pamoja na kanuni na kuruhusu mawazo tofauti.


Katika hotuba yake, Kinana alisema kanuni za wabunge wa CCM ambazo zilitungwa miaka 20 iliyopita, zinahitaji kuboreshwa kulingana na mahitaji ya wakati wa sasa.


Kinana hakutaja kanuni zilizopitwa na wakati, lakini mwaka jana baadhi ya wabunge wa CCM walionekana kuilaumu Serikali yao wakidai walikamatwa au kunusurika kutekwa saa chache kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu mjini Dodoma.


Pia baadhi wamelalamikia vikao vya vyama bungeni wakidai kuwa vinaua hoja binafsi za wabunge, wakati mfumo wa uendeshaji wa vikao hivyo pia unalalamikiwa kutokana na kuongozwa na Waziri Mkuu, ambaye ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni na hivyo wabunge kushindwa kuwa huru kutoa maoni yao.


“Hatuwezi na kwa kweli, itakuwa ni kasoro kubwa kudhani tutakuwa na chama au Serikali ambayo watu wote wanafikiri sawa, wana maoni sawa na wana kauli sawa katika kila jambo,” alisema Kinana ambaye amekuwa katibu mkuu wa CCM kwa miaka sita kuanzia mwaka 2012.


“Tukiwa na watu wa aina hiyo watakuwa ama hawafikiri au si wa kweli na tusiruhusu tofauti za mawazo na maoni sababu au chanzo cha mgawanyiko ndani ya chama au bungeni.”


“Isiwe nani zaidi bali iwe ni nani ana hoja nzito zaidi na zenye manufaa kwa maendeleo ya Taifa letu. Jambo la msingi hapa ni kujenga utayari wa kila upande kujitahidi kuelewa, kutafakari na kuheshimu hoja za upande mwingine.”


Kinana pia alisema ili CCM iendelee kushinda ni wajibu wa kila mwanachama kuendeleza sera za chama alizozielezea kuwa ni nzuri, kuwa karibu na wananchi, kuwasikiliza na kutimiza matarajio yao.


“Tutambue wapi tuchukue hatua kutatua matatizo yanayowakabili, yanayowasumbua na yanayowaudhi ili kuwafanya wasipoteze mapenzi na imani kwa chama chetu na kwa Serikali zetu,” alisema.


“Wametuamini na kutuchagua kwa imani kubwa na kwa matarajio makubwa. Tuwasikilize na tufanye hivyo kwa unyenyekevu na kwa wakati wote.”


Kinana alitaja mambo matatu ambayo CCM inapaswa kuyafanya ili kuendelea kujenga imani kwa wananchi.


“Kutimiza ahadi zetu kwa Watanzania kama zilivyo katika ilani, kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani na kujiandaa na uchaguzi mkuu ujao,” alisema Kinana.


Kinana alitumia fursa hiyo kuwaomba radhi wabunge kwa mapungufu yaliyojitokeza wakati akiwa katibu mkuu.


“Na kama kuna mafanikio yaliyopatikana basi yatakuwa hayakutojana na maarifa au juhudi zangu pekee, bali ni matokeo ya juhudi za wana CCM wote na jumuiya zake katika ngazi zote,” alisema.




Alichosema Majaliwa


Awali, mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge wa CCM, Kassim Majaliwa alimhakikishia Kinana kuwa yuko salama katika maisha yake ya kustaafu.


Alisema ushirikiano uliopo baina ya wabunge wa chama hicho ni nguzo ya ushindi wa chaguzi na kumhakikishia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwakani wataibuka kidedea na kumuhakikishia ushirikiano Dk Bashiru.


“Katibu Mkuu Bashiru Ally tunataka kukuhakikishia kwamba, utekelezaji wa ilani, maendeleo, kura huko chini ni ushirikiano wa wabunge na ili tushinde jitihada za mbunge ni kubwa sana na tunataka kukuhakikishia hatuko tayari kupoteza kiti chochote katika maeneo yoyote yale,” alisema Majaliwa.


“Uko hali salama, tutakulinda na tutakusemea, na wabunge wako tayari kukupigania.”


Alisema CCM itashinda uchaguzi wa serikali za mitaa kutokana na ushirikiano uliopo.


“Tunamshukuru Abdulrahman Kinana tumeweza kufanya naye kazi kwa weledi, jitihada na kwa mafanikio makubwa na amefikia wakati amestaafu na kurudi nyumbani kupumzika, anabaki kuwa mwanachama mtiifu,” alisema.


Naye mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, ambaye alizungumza kwa niaba ya wabunge vijana, alimshukuru Kinana kwa kazi aliyoifanya na kwamba alikuwa mlezi wa vijana.


“Nami nikuombe katibu mkuu mpya tuendelee kufanya kazi na kutulea vijana. Vijana ni moto kidogo, kusiwe na aina moja ya adhabu na bahati nzuri kumetoa aina ya kuadhibu na niwaombe viongozi tuzitumie adhabu zile ambazo ziko katika Katiba,” alisema.


“Kinana alitembea kila sehemu na Kinana alikwenda kijiji kule Kigoma ambacho hakijawahi kutembelewa na kiongozi yoyote toka uhuru. Kinana alikwenda kwa sababu ya mapenzi mema na chama na nikushukuru sana.”


Akimgeukia Dk Bashiru, mbunge huyo alimsifu kuwa amebobea katika siasa na hivyo atakisaidia chama hicho.




Wabunge wasingekubali


Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Wabunge wa CCM, Margaret Sitta ambaye ni mbunge wa Urambo alisema kama wangeulizwa bungeni, wanaosema Kinana astaafu, wengi wangekataa.


“Ulitupenda, ulitutetea na ulikuja kwetu na kutusikiliza. Kinana ulikipenda chama na kama mtakumbuka alipokuwa katibu mkuu alikitumikia chama kwa moyo wote na alipopata ukatibu mkuu alizunguka nchi nzima, alichangamsha chama ndiyo ukweli wenyewe,” alisema Sitta.
Na  Ibrahim Yamola, Mwananchi
CHANZO- MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527