SUGU : NASUBIRI RIPOTI YA DAKTARI KUHUSU AFYA YA MAMA KWENDA BUNGENI

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi maarufu Sugu ambaye tangu juzi yupo uraiani baada ya kutoka gerezani kwa msamaha wa Rais John Magufuli, amesema ataanza kushiriki vikao vya Bunge la bajeti mjini Dodoma baada ya kujua maendeleo ya afya ya mama yake mzazi.


“Nasubiri ripoti ya daktari kuhusu hali ya mama ndipo niweze kwenda bungeni. Ripoti hiyo huenda ikatolewa Jumapili (kesho),” amesema Sugu ambaye alikuwa akitumikia kifungo cha miezi mitano jela pamoja na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga

Bunge la bajeti lilianza Aprili 3, 2018 na linatarajiwa kumalizika Juni 30,

Sugu na Masonga walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela Februari 26 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli kwenye mkutano wa hadhara walioufanya Desemba 30 mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Wawili hao wameshatumikia adhabu hiyo kwa siku 73 ikiwa ni zaidi ya robo ya kifungo chao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527