RC KIGOMA AKABIDHI VYOO VYA KISASA, ATOA TAHADHARI KWA WAKUU WA WILAYA


Mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia jenerali Emmanuel Maganga, amewataka wakuu wa wilaya, watendaji na watumishi wa idara ya afya kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama Ebola pamoja na kuweka uangalizi katika mipaka kuzuia ugonjwa huo usiingie katika mkoa wa Kigoma. 

Maagizo hayo aliyatoa leo katika kikao cha kujadili na kupanga mikakati juu ya njia bora ya kuzuia kuingia kwa ugonjwa wa ebola kutokana na ugonjwa huo kuripotiwa kuwepo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Mkoa huo kuwa na muingiliano wa wafanya biashara kutoka nchi hiyo na wengine kwenda kwa ajili ya biashara kuweza kusababisha ugonjwa huo kuingia kwa urahisi nchini.

Akiwa katika kikao hicho pia amekabidhi vyoo vya kisasa 756 kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani humo ambavyo vitakavyopelekwa shuleni na katika vituo vya afya kwa lengo la kuepusha na ugonjwa wa kipindupindu.

Alisema hatamvumilia mkuu wa wilaya yeyote au mtumishi wa afya atakayekuwa sababu ya kuingia kwa ugonjwa huo kwani mkoa wa Kigoma umekuwa ukikumbwa na magonjwa mengi ya mlipuko kama kipindupindu ambapo umekuwa ugonjwa mkubwa mkoani humo.

Alisema endapo  kutabainika kuna ugonjwa wa mlipuko katika wilaya basi mkuu wa wilaya atachukuliwa hatua.

"Wakuu wa wilaya kazi yenu kubwa ni kutoa elimu kwa wananchi na kuwachukulia hatua watendaji wa afya wasiofanya kazi zao kikamilifu ambao wanasababisha magonjwa hayo kuingia nchini, ni wakati wa kuanza kukagua vyoo katika vijiji vyenu na kuwahamasisha wananchi kujiepusha kuingiliana na watu ambao wana magonjwa ya mlipuko... hatuko tayari kila siku sisi tunaongoza kwa mambo mabaya hatuwezi kuendelea bila kuwa na afya bora lazima afya izingatiwe", alieleza.

Aidha mkuu huyo alisema hayuko tayari kuona wananchi wanashindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa ya milipuko kwa kuwa kazi kubwa ya viongozi ni kuwahudumia wananchi na wananchi wasimamiwe kuzuia magonjwa ya milipuko na hakuna haja ya mkoa wa Kigoma kuwa masikini lazima juhudi zifanyike kuhakikisha mkoa unakuwa salama.

Nae afisa afya mkoa wa Kigoma Kulwa Makono alisema katika mikakati ya mkoa wameandaa fedha zitakazotolewa kwa wakuu wa wilaya kwa ajili ya kukagua vyoo katika vijiji na wameleta vyoo ambavyo vinazuia harufu mbaya.

 Alisema wameandaa vyoo zaidi ya 756 kwa aajili ya shule na vituo vya afya kwa ajili ya kuzuia magonjwa ya milipuko kama pipindupindu.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Petter Nsanya kwa niaba ya mganga mkuu wa mkoa alisema,Ebola ni ugonjwa ambao unasambazwa na virusi vinavyoitwa ebola na ugonjwa huo ulianzia nchini Congo mwaka 1976 na waligundulika wagonjwa 318 wagonjwa na waliofariki ni wagonjwa 248 walipoteza maisha.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia jenerali mstaafu Emanuel Maganga akimkabidhi choo cha kisasa Mkurugenzi wa halmashauri ya  Kibondo Juma Mnwele kwa niaba ya wakurugenzi wenzake ambacho ni  kati ya vyoo 756 vitakavyopelekwa shuleni na katika vituo vya afya kwa lengo la kuepusha na ugonjwa wa kipindu pindu- Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527