MBUNGE WA CCM AMWAGA MACHOZI BUNGENI

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Jacqueline Ngonyani ‘Msongozi’ ametoa chozi bungeni akiitaka Serikali kuwalipa mawakala wa pembejeo na kuacha kutumia kivuli cha uhakiki wa madeni hayo kutoyalipa.


Akichangia bajeti ya kilimo, jana Mei 15, 2018 bungeni, Msongozi amesema madai hayo yamedumu kwa zaidi ya miaka minne huku baadhi wakifariki kabla hawajalipwa.


“Nashangaa sana mawakala wa pembejeo wanadai miaka minne, walihudumia wakulima wetu na walikwenda kukopa fedha katika taasisi, ambazo sasa zinawadai,” amesema Msongozi.


Huku akishangiliwa na wabunge, Msongozi amesema, “Serikali imekuwa inajificha katika kichaka cha uhakiki, kwa nini hawawalipi? Serikali imekwenda kujificha katika uhakiki, ni uhakiki wa aina gani? Kuna watu wanakufa bila kupewa fedha zao.”


Msongozi akizungumza kwa sauti yenye kuashiria kulia huku mkono wake akiupeleka kufuta uso wake, amesema, “katika nchi hii watu wanatafuta haki zao, kama wameiba kwa nini wasipelekwe mahakamani, kwa nini hawapewi fedha zao, uhakiki gani, mbona watumishi siku mbili walihakikiwa? Kwa nini huku katika mawakala hawalipwi fedha zao.”


Amesema kuna kijana alitaka kujinyonga kwa kudaiwa na taasisi jambo ambalo amesema Serikali ichukue hatua ya kulipa madai kwani wako mawakala saba wamepoteza maisha.”


Msongozi amekuwa mbunge wa tatu kutoka CCM kutokuunga mkono bajeti hiyo akitanguliwa na Richard Ndassa (Sumve) na Mashimba Ndaki (Maswa Magharibi).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527