MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU APOKEA VIFAA VYA UPASUAJI KWA WATOTO KUTOKA KUWAIT

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.


Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) jana tarehe 15 Mei, 2018.


“ Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.


Makamu wa Rais alisema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.


Makamu wa Rais amlisema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.


Wakati huo huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.


Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem alisema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527