DNA SASA KILA MKOA


Moja ya majukumu maarufu zaidi ya GCLA ni upimaji wa uwiano wa vinasaba vya binadamu, maarufu DNA, hivyo huduma hiyo kufanyika mikoani pia badala ya ngazi ya kanda kama ilivyo sasa.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa mkutano wa baraza la wafanya kazi wa GCLA, wenye lengo la kujadili utekelezaji wa majukumu yake.

Dk. Mafumiko alisema kwa sasa maabara ziko katika kila kanda nchini, katika mpango wake wa muda mrefu anatarajia kuanzisha ofisi katika kila mkoa nchini.

Alisema ofisi yake inatarajia pia kununua mitambo, mashine za kisasa na vifaa vya teknolojia ya kisasa vitakavyorahisisha utekelezaji wa majukumu ya maabara zilizopo katika kanda zote nchini.

"Katika kipindi cha mwezi mmoja niliokaa katika ofisi hii, nimeona niweke kipaumbele katika kupanua utoaji wa huduma za maabara zetu katika kila mkoa ambao ni mpango endelevu, lakini pia kununua mashine na mitambo yenye teknolojia ya kisasa," alisema.

Alisema mipango hiyo ina lengo la kusogeza huduma karibu na jamii katika mikoa mbalimbali badala ya kutegemea maabara ya makao makuu.

"Kutokana na dunia inavyobadilika kila siku ni vyema kuwa na vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha utekelezaji wa majukumu yetu kwa haraka na kwa teknolojia ya hali ya juu, lakini pia jamii ipate huduma mikoani badala ya kusafiri kufuata maabara ya jijini Dar es Salaam," alisema.

Kadhalika, aliwataka watumishi wa maabara hiyo kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa sababu ya umuhimu na wajibu walionao kwa taifa.

"Kila mtumishi wa mamlaka hii muhimu atambue nafasi ambayo taifa limetupa na linatuamini. Weledi na uaminifu ni muhimu kwa ofisi yetu. Tutakapofanya vizuri tutakuwa tumewatendea haki Watanzania na Mheshimiwa Rais (John Magufuli), ambaye ameiweka mamlaka hii," alisema na kuongeza;

"Pia ni muhimu kuzipitia sheria zetu zinazotuongoza kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yetu na kuzisaidia mamlaka nyingine kutenda haki."

Awali kabla ya kufungua mkutano huo wa kwanza tangu taasisi hiyo kuwa mamlaka kamili, Dk. Mafumiko alisema lengo ni kujadiliana hoja za wafanyakazi, taarifa ya bajeti ya fedha ya mwaka 2018/19 na utekelezaji wa majukumu ya maabara hiyo.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Mohamed Kambi, ambaye alifungua mkutano huo, aliwataka wafanyakazi hao kuibua hoja zitakazojenga na kuimarisha utekelezaji wa mamlaka hiyo badala ya kulalamika.

Pia alimtaka Mkemia Mkuu wa Serikali kutumia watumishi wa mamlaka hiyo kama nyenzo muhimu ya kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527