DAWA YA KUTIBU UPARA YAPATIKANA...SASA WENYE UPARA KUCHEKELEA


Dawa ya kutibu upara imegunduliwa ambayo inatumia dawa ya kutibu mifupa iliyodhoofika.

Watafiti wamegundua kupitia maabara kwamba dawa hiyo ina athari kubwa katika mashina ya nywele kwa kuzipatia nguvu nywele na hivyo kuziwezesha kumea.

Dawa hiyo inashirikisha vipengele vinavyolenga protini ambayo hutumika kuzuia umeaji wa nywele na hivyo kusababisha upara.

Kiongozi wa mradi huo, Dk. Nathan Hawkshaw kutoka Chuo Kikuu cha Manchester anasema ugunduzi huo unaweza kuleta tofauti kwa watu wanaokabiliwa na tatizo la ukosefu wa nywele.

Kabla ya ugunduzi huu, ni dawa mbili pekee ambazo zimekuwa zikitumika kutibu upara. Dawa hizo ni minoxidil, kwa wanaume na wanawake na finasteride, kwa wanaume pekee.

Dawa zote mbili zina madhara na hukosa kufanya kazi mara nyingine na ndiyo maana watu wenye tatizo la upara hupendelea kufanya upandikizaji wa nywele badala yake.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la PLOS Biology ulifanywa kwenye maabara, huku sampuli zikiwa na nywele kutoka kwa zaidi ya wagonjwa 40 wa kiume wanaotaka kupandikizwa nywele.

Dk. Hawkshaw aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC kwamba jaribio litafanywa kuona iwapo tiba hiyo inafanya kazi na ni salama kwa watu.

NINI KINACHOSABABISHA KIPARA?

Kupotea kwa nywele ni suala la kila siku na sio tatizo la kumtia mtu wasiwasi. Baadhi ya nywele huwa ni za kudumu huku nyingine zikiwa za muda mfupi.

Msemaji wa Muungano wa Madaktari wa Ngozi nchini Uingereza, aliiambia BBC kwamba utafiti huu ni muhimu sana kwa afya ya wengi:

“Watafiti wanasema kuwa kupotea kwa nywele ni tatizo la kawaida na linaweza kuathiri afya yako ikiwa ni pamoja na kukosa kujiheshimu na kujiamini…Hata hivyo, utafiti zaidi utahitajika kufanywa kabla ya kutumika kwa watu walio na tatizo la kupoteza nywele.”

Pamoja na yote kwa watu wenye tatizo la kupotea kwa nywele, tiba imepatikana.

Hatua hiyo inawapatia waathiriwa afueni kwa kuwa kuna chaguo la dawa ambazo zinaweza kutibu.

Chanzo: BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527