WANAUME WAPEWA ELIMU KUTOKOMEZA MILA NA DESTURI KANDAMIZI KUPIGA VITA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI KISHAPU

Meneja mradi wa kutokomeza mila na desturi kandamizi kutoka Shirika la Agape mkoani Shinyanga Peter Amani akitoa elimu kwa baadhi ya wanaume wilayani Kishapu namna ya kutambua majukumu yao katika familia na kuachana kabisa kuendekeza mila na desturi ambazo zilishapitwa na wakati, ili kumaliza tatizo la mimba na ndoa za utotoni wilayani humo.


****
Shirika la Agape mkoani Shinyanga limetoa elimu ya kuwajengea uwezo wanaume wilayani Kishapu mkoani hapa namna ya kupambana kutokomeza mila na desturi kandamizi ambazo zimekuwa kichocheo kikubwa cha kushamiri kwa mimba na ndoa za utotoni.

Shirika hilo linatekeleza mradi wake wa kutokomeza mila na desturi kandamizi wilayani Kishapu kwa muda wa miaka miwili, kuanzia (2017-2019) kwa ufadhili wa Shirika la Save The Children, ambapo mradi huo unatekelezwa kwenye kata 12 wilayani humo, kwa lengo la kumaliza matukio ya mimba na ndoa za utotoni.

Elimu hiyo ya kuwajengea uwezo wanaume hao imetolewa  Februari 26,2018 katika kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu na kukutanisha baadhi ya wanaume kutoka kata za Ngofila, Talaga, Itilima, Kiloleli, Lagana, na Mwamashela, ambapo Februari 27,2018 watatoa elimu hiyo hiyo katika Kata za Somagedi, Bunambiu, Mwamalasa, Shangihilu, Masaga na Mwakiponya.

Akizungumza wakati akitoa elimu hiyo Meneja mradi huo wa Shirika la Agape Peter Amani, alisema idadi kubwa ya wanaume wilayani humo hawana elimu ya kuacha kuendekeza mila na desturi kandamizi zilizopitwa na wakati na hivyo kusababisha kuendelea kukithiri kwa matukio ya mimba na ndoa za utotoni.

“Mila na desturi hizi kandamizi zimekuwa kikwazo kikubwa kwenye suala la kupambana na matukio ya mimba na ndoa za utotoni wilayani Kishapu, na ndiyo maana tumeamua kutoa elimu hii kwa wanaume ambao wao ndio vichwa vya familia na wamekuwa wakiziendekeza, na kusababisha kuzima ndoto za wanafunzi,”alisema. 

"Elimu ambayo tunaitoa hapa ni wanaume kutambua majukumu yao katika kuhakikisha mila na desturi kandamizi zinatokomea ndani ya jamii, kusomesha watoto, kuacha kuwarubuni wafanye vibaya kwenye mitihani yao, pamoja na kuacha kuwaogesha dawa za mapenzi (Samba)”,aliongeza. 

Naye mmoja wa wanufaika wa elimu hiyo Abasi Masanja, alilipongeza shirika hilo kwa kutoa elimu hiyo ambapo wanaume wengi walikuwa gizani hususani kwenye suala la kuwekeza watoto wao kwenye elimu, na kuahidi kuondokana na mila na desturi hizo kandamizi, mara baada ya kupata upeo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola, akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo aliwataka wanaume hao pia kuondokana na mila na desturi za kutoshirikisha wake zao kwenye masuala ya kifamilia, likiwemo la kuuza mavuno ambapo wanaume wengi wamekuwa wakiyauza na kisha kutokomea kwenda kufanya anasa.

Alisema pindi watakapouza mavuno hayo wakae na familia zao kupanga mipango ya maendeleo, ikiwemo kujenga nyumba za bati na kuondokana na matembe, kununua mifugo jambo ambalo litatokomeza tamaa ya kuozesha wanafunzi kwa lengo la kupata ng’ombe, pamoja na kujikita kusomesha watoto wao. 
Mmoja wa wanaume waliojengewa uwezo Abasi Masanja, akiwasilisha mada kwenye kikundi chake juu ya athari za kuendekeza mila na desturi Kandamizi, kuwa zina sababisha kukosa malezi mazuri kwa mtoto wa kike, sababu ya kutothaminiwa tofauti na mtoto wa kiume, na kujikuta wakikatisha ndoto zake na kuozeshwa ndoa za utotoni kwa tamaa ya kupata mifugo,pia kunyima mwanamke fursa ya kuchangia mawazo ya kimaendeleo ndani ya familia na kujikuta wakiendelea kuwa maskini. 
Simoni Nkende akiwasilisha mada kwenye kikundi chake amesema mila na desturi kandamizi zimekuwa tatizo kwenye mfumo mzima wa kimaendeleo, na hata kwenye ukuaji wa kiuchumi kutokana na kuwa na mawazo mgando na hivyo kujikuta wakiharibu ndoto za watoto wao kwa kuwakatisha masomo na kuwaozesha katika umri mdogo kwa tamaa ya kupata mifugo na mali.
Hassani Jafari akichangia mada kwenye kikao chao cha kujengewa uwezo wa kutokomeza mila na desturi kandamizi na kubainisha moja ya changamoto ambayo imekuwa kikwazo kwenye tatizo la kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ni Sheria ya ndoa ya Mwaka (1971) ambayo imekuwa ikiruhusu mtoto aliye chini ya umri wa miaka 14 na 15 ana ruhusiwa kuolewa kwa idhini ya wazazi wake au mahakama, na hivyo kuiomba serikali iitengue sheria hiyo ambayo imekuwa mwiba kwao, hususani pale wanapo kamatwa watuhumiwa ambapo sheria hiyo imekuwa kinga kwao.
Mkurugenzi wa Shirika la Agape John Myola akiwataka wanaume hao kuacha tabia ya kuogopa lawama bali wawe majasiri na kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola au viongozi wa serikali za mitaa, hususani pale wanaposikia mtoto wa fulani anataka kuozeshwa, na siyo kukaa kimya kitendo ambacho hakitamaliza tatizo la mimba na ndoa za utotoni wilayani Kishapu.
Baadhi ya wanaume walioshiriki elimu hiyo ya kutokomeza mila na desturi kandamizi wakiendelea kusikiliza elimu kutoka kwa viongozi wa Shirika hilo la Agape, na kutakiwa wakawe mabalozi kwa wenzao ambao hawakufika kwenye elimu hiyo ili kuwa kitu kimoja katika suala zima la kupambana na tamaduni ambazo zilishapitwa na wakati na kuharibu ndoto za wanafunzi.
Wanufaika wa elimu ya kutokomeza mila na desturi kandamizi, wakiendelea kusikiliza na kutafakari juu ya athari ambazo husababishwa na kuendekeza Mila hizo ambazo ndio chanzo kikuu cha kukithiri kwa tatizo la mimba na ndoa za utotoni, ikiwamo mila ya kuogesha watoto dawa ya mapenzi (Samba), ili wapate kupendwa na wanaume kwa tamaa ya kuwaozesha na kupata mifugo, na kujikuta watoto hao wakiambulia mimba na ndoa za utotoni, na kuishi maisha ya shida mara baada ya kushindwa kuhudumia majukumu ya kifamilia, sababu wanakuwa bado hawajakomaa kiakili,kiafya na kimwili, na wengi wao hujikuta miji ikivunjika na kukimbilia miji kutafuta maisha, na kuishia kufanya kazi za ndani au kufanya biashara ya kuuza mili yao.
Wanufaika wa elimu hiyo wakiwa kwenye makundi na kupanga mipango kazi ambayo wataifanya mara baada ya kupata elimu hiyo ya kutokomeza mila na desturi kandamizi, kuwa watakuwa wakikaa na mabinti zao na kuwaeleza juu ya madhara ya kuwa na mahusiano katika umri mdogo, na kuwa asa juu ya umuhimu wa kupenda elimu na faida zake.
Wanakikundi wakiendelea kujadili na kupanga mpango kazi ambao utatokomeza mila na desturi kandamizi ndani ya jamii na kuwafanya akina mama na watoto kuishi salama.
Wanakikundi wakiendelea na upangaji wa mipango kazi ya kutokomeza mila na desturi kandamizi zilizopitwa na wakati, na kupanga kwenda kutoa elimu ya kuacha suala la ukeketaji wa watoto wa kike, hususani kwenye kata ya Mwamalasa wilayani humo ambapo asilimia kubwa wanaishi kabila la Wataturu.
Picha kwa hisani ya Shinyanganews blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527