MAGUFULI AMWAGA BILIONI 200 KULIPA MADENI YA NDANI


Rais John Magufuli amesema, mwezi ujao Serikali itatoa Sh bilioni 200 kwa ajili ya kulipa madeni ya ndani yatakayokuwa yamehakikiwa yakiwemo ya wazabuni mbalimbali waliotoa huduma katika taasisi za serikali, madai ya walimu na madai ya wakandarasi.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo, wakati alipokuwa akiagana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu leo Ikulu, jijini Dar es Salaam.

“Nasisitiza madeni tutakayolipa ni ya ndani, na tutalipa madeni ambayo yamehakikiwa, kwa hiyo maandalizi ya kutoa fedha hizo yaanze mara moja na ni matarajio yangu fedha hizi zitasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wetu” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amempongeza Profesa Ndulu kwa utumishi wake wa miaka 10 na kazi nzuri aliyoifanya ya kusimamia uchumi ambapo katika kipindi hicho kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kwa wastani wa asilimia 5 hadi asilimia 7 na kuimarisha usimamizi wa benki na maduka ya kubadilishia fedha.

Mengine ni kusimamia ongezeko la akiba ya fedha za kigeni inayoiwezesha nchi kumudu kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi sita na kuanza kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme, ununuzi wa ndege na mingine.

“Nakushukuru sana Prof. Ndulu, umefanya kazi nzuri ya kusimamia uchumi wa Taifa letu, ndio maana leo unamaliza muda wako lakini tayari Benki ya Dunia na kamisheni ya dunia inayoshughulikia teknolojia na maendeleo shirikishi wanakuhitaji ufanye nao kazi, na mimi nimeidhinisha uende ukatuwakilishe” amesema.

Prof. Ndulu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kufanya nae kazi tangu alipoingia madarakani na amebainisha kuwa anafurahi kumaliza kipindi chake huku uchumi wa nchi ukiwa mzuri.

Aidha, amempongeza Rais Magufuli kwa miongozo muhimu iliyosaidia kuimarisha uchumi ikiwemo kudhibiti mfumuko wa bei ambao mwezi Novemba 2017 ulifikia asilimia 4.4 na kuongezeka kwa akiba ya fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.8 hadi kufikia Dola za Marekani Bilioni 6 hivi sasa, hali ambayo imeimarisha uwezo wa Serikali kujiendesha na kugharamia miradi mikubwa ya maendeleo.

“Nimekuja kumuaga Mhe. Rais na kumshukuru, nafurahi kuwa naondoka wakati hali ya uchumi ikiwa nzuri, Taifa linakopesheka na kuna mazingira mazuri zaidi ya uchumi kuendelea kukua, nampongeza sana Rais kwa kusimamia mambo mbalimbali muhimu ya kuimarisha na kukuza uchumi katika kipindi chote nilichofanya nae kazi” amesema Prof. Ndulu.

Rais Magufuli pia amezungumza na kumpongeza Gavana Mteule Profesa Florens Luoga kwa kupokea uteuzi wake na amemtaka kufanya kazi ya kusimamia uchumi wa Taifa kwa ufanisi mkubwa zaidi ili nchi ipige hatua za maendeleo kwa kasi zaidi.

Baada ya mazungumzo hayo, Prof. Luoga amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uteuzi huo na kumhakikishia kuwa ataisimamia BoT ili iendelee kuwa chombo imara cha kusimamia uchumi wa nchi, kuisimamia fedha ya Tanzania na kuhakikisha nchi inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na mradi wa umeme katika maporomoko ya maji ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

Prof. Luoga ameungana na Prof. Ndulu kueleza kuwa taarifa zinazotolewa na BOT kuhusu ukuaji wa uchumi zinaandaliwa kitaalamu na kwa kushirikisha vyombo mbalimbali vikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na ameonya dhidi ya baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu takwimu za uchumi zinazotolewa na BOT.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527