CCM YAMSAKA MCHAWI WAKE ALIYEIPA KURA UKAWA UCHAGUZI WA MEYA DAR

Wajumbe wa CCM wanaoingia kwenye Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam, wamesema wapo katika hatua za mwisho za kumpata mjumbe mwenzao aliyesababisha wao kushindwa uchaguzi wa naibu meya wa jiji hilo.


Uchaguzi huo uliokuwa na mchuano mkali kutokana na kila upande kuwa na wajumbe kumi na moja, ulifanyika juzi katika ukumbi wa Karimjee na Mussa Kafana wa CUF akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) aliibuka kidedea kwa kupata kura 12 dhidi ya 10 alizopata Mariam Lulida wa CCM.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mjumbe baraza hilo CCM, Abdallah Chaurembo alisema tayari wanao ushahidi na wameshaanza kumbaini mjumbe ambaye alisababisha chama chao kushindwa katika uchaguzi huo.


“Tunataka kuirahisishia kazi kamati ya siasa ya mkoa kwa kumpata kwanza mjumbe huyu, halafu wao ndiyo watakaokuwa na jukumu la kumtangaza na kumchukulia anazostahili kwa mujibu wa makosa yake,” alisema Chaurembo.


Chaurembo ambaye pia ni Meya wa Temeke alisema walishaanza kumbaini mjumbe huyo kabla ya kazi ya kuhesabu halijakamilika na kudai kwamba hakuwa na nia ya dhati na CCM.


“Tulishakijua alichokuwa akikifanya, kwanza alikuwa anatetemeka wakati anaenda kupiga kura. Wakati yupo katika eneo la kupiga yeye ndiyo alitumia takriban dakika tano wakati wenzake nusu dakika.


“Hivi mtu unachukua takriban dakika tano nzima katika kupiga kura, una nini wewe, ina maana hujui kusoma wala kuandika? Alihoji Chaurembo. Nawaambia WanaCCM tutampata mtu huyo very soon (muda mfupi).


Alisema wameamua kushughulikia jambo hilo, ili iwe funzo kwa madiwani wengine wasiokitakia mema chama hicho na kwamba, hiyo itakuwa njia ya kuwaondoa wale viongozi wasio na masilahi na CCM.


Alieleza kuwa wajumbe wa CCM katika baraza hilo, wana imani wameshindwa katika uchaguzi kwa hoja mbili ambazo ni Ukawa kutumia utemi wakati kura mbili ziliharibika, na mjumbe mwenzao kuharibu kura na siyo kumpigia kura mgombea wa upinzani.


Katika uchaguzi huo, Chaurembo na meya mwenzake wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob nusura wazichape wakati wa shughuli ya kuhesabu kura kama si wajumbe wa uchaguzi huo kuwatenganisha.


Chaurembo aliendelea kwa kufafanua kuwa mjumbe huyo akishapatikana wajumbe wa CCM wa baraza ndiyo watakaokuwa mashahidi kwenye kamati ya siasa ya mkoa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527