WANAUME MOROGORO WALALAMIKA KUNYANYASWA NA WAKE ZAO


Watu wapatao 174 wakiwemo wanaume 86 wamefanyiwa matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Taarifa hiyo ni ya kipindi cha mwaka 2016 hadi Novemba 30, mwaka huu. 

Imeelezwa kuwa wanaume hao wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya karaha katika ndoa zao kwa namna ambavyo haiswihi.

Ufafanuzi zaidi katika ukatili dhidi ya wanaume umeelezwa kuwa upo katika masuala ya unyumba zaidi na hasa wanapokuwa wamekosa uwezo wa kutunza vyema familia zao kwa sababu zozote zile za kijamii.

Pamoja na manyanyaso hayo kwa wanaume imeelezwa kuwa kuna changamoto kubwa za mimba za utotoni pamoja na tabia zingine za kikatili dhidi ya wanawake na wanaume.

 Taarifa hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohamed Utaly juzi alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Dakawa wilayani humo, ikiwa ni mwendelezo wa siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Kampeni hiyo imeandaliwa na kituo cha wasaidizi wa kisheria wilaya ya Mvomero pamoja na Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria Morogoro (MPLC).

 Akikariri taarifa iliyowasilishwa kwake na Idara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alisema wanawake 88 na wanaume 86 wakiwemo watoto wa kike ndio waliopata manyanyaso hayo ikiwamo ndoa na mimba za utotoni.

Kutokana na taarifa hiyo mkuu huyo wa wilaya, aliwataka watendaji idara za afya na ustawi wa jamii katika halmashauri ya wilaya hiyo kuchukua hatua za haraka kumaliza matukio hayo.

 Ili kukabiliana na changamoto za mimba za utotoni, serikali ya wilaya hiyo imesema iko kwenye utaratibu wa kujenga hosteli kwa wanafunzi wa shule sekondari kwa lengo la kuwakinga na vishawishi.

IMEANDIKWA NA JOHN NDITI - HABARILEO MVOMERO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527