WAKULIMA 2000 WA ALIZETI WAPATIWA MBEGU BURE KAHAMA

Zaidi ya wakulima 2,000 wanachama wa chama cha ushirika cha Ibuka Multipurpose Co-operative Society Ltd kati ya 4,772 wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamepatiwa mbegu za zao la alizeti ili kulima mbadala wa mazao ya biashara kama vile pamba ambayo imekuwa na changamoto nyingi za uzalishaji wake.

Hayo yameelezwa juzi wilayani Kahama mkoani Shinyanga na meneja mkuu wa ushirika huo Musiba Mkama wakati wa hafla fupi ya ufunguzi wa jengo la kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti cha ibuka oil mill ambapo alisema wakulima hao elfu 2 wamepewa mbegu hizo kila mmoja kilo 2 huku lengo ni kuwapatia wote bure wanachama 4,772.

Mkama alisema hali hiyo ya kuwawezesha wakulima hao wanachama wa ushirika huo ni moja ya mikakati ya kupata mali ghafi itakayotumika kwenye kiwanda hicho kwa kuwa baada ya alizeti kuvunwa ushirika huo ndiyo utakaowanunulia ambao pamoja na kiwanda kukiwezesha kufanya kazi pia itasaidia kuinua uchumi kwa wananchi.

Kabla ya hapo mwenyekiti wa ushirika huo Raphael Buhulula alisema pamoja na kuwanunulia alizeti wakulima hao pia wametenga hekali 500 za ushirika ambao watalima zao hilo ili kuendelea kukiwezesha kiwanda kufanya kazi.

Buhulula alisema mwaka jana walilima hekali 35 lakini kutokana na hali mbaya ya msimu wa mvua waliweza kupata mavuno ya magunia 208 ambayo tayari ndio yatakuwa ya kuanzia kwenye kiwanda hicho ambacho mpaka kukamilika kitagharimu zaidi ya milioni 90.

Naye mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Shose Monyo aliwataka viongozi hao kuwa makini ya kuingiza wanasiasa kwenye mambo ya ushirika kwani wanasiasa wakishaingia humo hawawezi kusonga mbele kama walivyoonesha mafanikio.

Shose alisema katika mkoa wa Shinyanga Ibuka ni ushirika mmoja wapo ulionyesha mafanikio makubwa kwa kujiendeleza wenyewe ikiwemo kuanzisha kiwanda hicho na kumiliki ardhi wanaoitumia kwenye kilimo na pia kuwa na vitendea kazi kama vile matrekta 3 na vifaa vyake vya kulima hali ambayo ni maendeleo makubwa ambayo wakiingiza siasa yanatoweka.

Na Shija Felician - Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527