SABABU ZA MAULID MTULIA KUJIUZULU UBUNGE NA UANACHAMA CUF NA KUHAMIA CCM


Mbunge wa Kinondoni jijini Dar, Maulid Mtulia (CUF)  ametangaza kujiuzulu ubunge na kujivua uanachama wa Chama cha Wananchi CUF na kuhamia CCM.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Mtulia amesema kuwa ameamua kufanya uamuzi huo Disemba 2,2017 kwa utashi wake bila shinikizo la mtu yeyote.

Mtulia ameelezea sababu za kujiuzulu nafasi yake hiyo ya ubunge na kuhama chama kuwa imetokana na uzoefu alioupata kwa miaka miwili ya ubunge, na kusema “nimebaini kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo sisi upinzani tuliahidi kuyatekeleza” alisema.

Aidha Mbunge huyo amesema kuwa nia yake ni kuwatumikia wananchi, na haoni sababu ya kuendelea kuwa upinzani na badala yake anaona ni vema aungane na juhudi za Serikali, kwa kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo na kukabiliana na kero mbalimbali.

Mtulia amesema anawashukuru wananchi wa Jimbo la Kinondoni, kwa kumpa dhamana ya ubunge, katika uchaguzi mkuu uliopita na amewaahidi kuwa yupo tayari kuendelea kushirikiana nao katika maendeleo, akiwa katika uwanja mwingine wa siasa ambao ni Chama Cha Mapinduzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527