MASHEHE WATANO WA BAKWATA WAJIUZULU UONGOZI MKOANI KATAVI


Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakari Zubeir

MASHEHE watano akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) Mkoa wa Katavi, Shehe Shaaban Bakari wamejiuzulu uongozi wakidai kuwepo kwa migogoro ya uongozi na ukiukwaji wa Katiba ya Bakwata.

Halmashauri ya baraza hilo inaundwa na viongozi sita ambao ni mashehe, watano kati yao ndio waliotangaza kujiuzulu ambao ni Mwenyekiti wao Shehe Bakari, Shehe Mashaka Kakulukulu, Shehe Hassan Mbaruku, Shehe Said Haruna Omary na Shehe Mohamed Sigulu.

Wakitangaza uamuzi huo jana mjini hapa mbele ya waandishi wa habari, Shehe Kakulukulu alisema haoni sababu ya kuendelea kuwa kiongozi wa halmashauri ya baraza hilo akidai kumekuwepo na baadhi ya mambo ya kimaendeleo hayaendi sawa.

“Hata Katiba ya Bakwata imekuwa ikikiukwa na kusababisha migongano ya kimaslahi, hata utekelezaji wa miradi ya maendeleo umekwama kutokana na msuguano wa kiuongozi,” alieleza Shehe Kakulukulu.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mashehe wengine, huku Shehe Sigulu akidai kuwa msuguano uliopo wa kiuongozi ndani ya Bakwata umesababishwa na mwalimu wa madrasa katika Msikiti Mkuu mjini Mpanda kuamua kuacha kazi ya kufundisha hivi karibuni.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527