KAKUNDA AMALIZA MGOGORO WA KUGOMBEA MAJENGO YA HALMASHAURI KAHAMA


Hatimaye sakata la kugombea majengo ya halmashauri ya Ushetu lililokuwa likifanywa na madiwani wa halmashauri mbili za Ushetu na mji limemalizika baada ya naibu waziri ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Joseph Kakunda kuyakabidhi majengo hayo.

Kabla ya hapo baraza la madiwani wa halmashauri ya Ushetu chini ya mwenyekiti wake Juma Kimisha lilipinga agizo la katibu mkuu Tamisemi Musa Iyombe la kutaka majengo hayo yakabidhiwe halmashauri ya mji Kahama baada ya Ushetu kuondoka kwenda makao makuu yake huko Nyamilangano umbali wa kilometa 72 kutoka Kahama mjini.

Awali mwaka 2012 halmashauri ya wilaya ya Kahama iligawanyika mara 3 na kuzaa Ushetu, mji Kahama na Msalala huku katika mgawanyiko wa mali Ushetu ambayo kabla hajabadili jina ilikuwa ndiyo halmashauri ya wilaya ya Kahama na ndiyo mama iliyozaa Msalala na mji hivyo ilibaki na majengo ya ofisi zote za wilaya.

Hata hivyo baada ya muda ilibadili jina na kuwa halmashauri ya Ushetu na makao makuu yake kuwa kule Nyamilangano na mwaka jana ilihamishia makao makuu yake huko hivyo majengo yaliyobaki mji Kahama Tamisemi kupitia katibu mkuu wake Iyombo iliagiza majengo hayo yakabidhiwe mji kwa kuwa wao wanabaki hali ambayo ilipingwa vikali na madiwani hao wa Ushetu.

Katika vikao vilivyotangulia vya baraza la madiwani chini ya mwenyekiti wao Kimisha walipinga vikali kuyakabidhi majengo hayo kwa madai ni mali yao pamoja na kuhama kuyaacha mjini Kahama lakini watayatumia kama sehemu ya kitega uchumi na vyanzo vya mapato ingawa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack aliagiza makabidhiano ya majengo hayo yasiingizwe wanasiasa wakiwemo wabunge na madiwani.

Kwa upande wake baraza la madiwani wa halmashauri ya mji wa Kahama chini ya mwenyekiti wake Abel Shija katika kikao kilichomalizika mwezi uliopita walimuagiza mkurugenzi wao Anderson Msumba kuhakikisha kwamba anafuatilia majengo hayo hasa kutokana na serikali kushindwa kuwapa fedha za ujenzi wa ofisi kwa madai hawawezi kupewa kutokana na wao kuwa na majengo mengi yaliyoachwa na Ushetu.

Kufuatia hali hiyo naibu waziri Kakunda alimaliza mgogoro huo kwa kuyakabidhi yeye mwenyewe majengo hayo kwa halmashauri ya mji Kahama bila kuwepo wanasiasa huku akiwatahadharisha kuwa majengo ya serikali huwa hayapangishwi kwa mtu binafsi anayefanya biashara na Halmashauri ikitaka kupangisha itapangisha majengo yake kwa tasisi za kiserikali kwa kibali toka kwa mkuu wa wilaya pamoja na katibu tawala wa mkoa.

Kakunda alisema mali zote zinazotumiwa na Halmashauri ni mali ya serikali na ndio maana hakuna Halmashauri inayojiendesha yenyewe kwa kutegemea mapato yake ya ndani nakuongeza kuwa kila mwaka serikali kuu inatoa ruzuku kwa kila halmashauri kwa ajili ya kujiendesha na kuwahudumia wananchi.

Naye mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu Michael Matomola alimtaka mkurungenzi wa halmashauri ya mji wa kahama kumwachia chumba kimoja kwa ajiri ya kutunzia mali zilizopo kwa kipindi cha miezi mitatu nakuongeza pindi watakapomaliza ujenzi wa makao makuu yao ya Ushetu kwa kipindi hicho watahamisha mali hizo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa kahama Anderson Msumba alisema kuwa kupatiwa majengo haya zitakuwa karibu idara zote na itakuwa rahisi katika kuwahudumia wananchi mwakani, kwani kwasasa idara za halmashauri zimegawanyika katika majengo mawili tofauti hali ambayo utowaji wa huduma ilikuwa ni changamoto kubwa.


Katika hatua nyingine Kakunda ameitaka Halmashauri ya Msalala kufikia tarehe 30/6/2018 kuhakikisha wanahamia katika makao makuu yao yaliyopo kata ya Ntobo Halmashauri ya Msalala hata kama ujenzi utakuwa haujakamilika kwa kuwa nayo kwa sasa inatumia ofisi ya sehemu za majengo hayo yaliyokabidhiwa halmashauri ya mji wa Kahama.

Na Shija Felician - Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527