MANULA, KICHUYA WAPEWA NJUMU ZA SH 500,000

NYOTA wawili wa kutumainiwa wa klabu ya Simba, Mlinda mlango Aishi Manula pamoja na kiungo mshambuliaji Shiza Kichuya, wamepokea viatu vyenye thamani ya Sh 500, 000 kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Wawili hao walikabidhiwa viatu hivyo aina ya CR7 Mercurial kutoka kampuni ya Nike, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Lipuli, ulioisha kwa sare ya bao 1-1 uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa viatu hivyo, Manula alisema anajisikia fahari kupata zawadi hiyo kutoka kwa mashabiki hao ambao wameonyesha upendo wao kwake na kuahidi kuendelea kufanya vizuri ili kuwafurahisha zaidi.

“Ni jambo zuri ambalo linatia hamasa ya kuendelea kujituma zaidi na kuisaidia timu kufanya vizuri zaidi katika michezo ya ligi kuu ili tuweze kutimiza malengo yetu,” alisema.

Naye Kichuya alisema zawadi hiyo itakuwa chachu kwake kufanya vizuri zaidi kutokana na upendo anaoonyeshwa na mashabiki hao, ambao wamekuwa wakiwaunga mkono katika harakati zao za kulisaka taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527