ODINGA : MITAMBO YA TUME YA UCHAGUZI IEBC ILIDUKULIWA...MATOKEO YANA ULAGHAI WA HALI YA JUU

Mgombea urais wa muungano wa upinzani Nasa Raila Odinga amewaambia wanahabari kwamba wamepata habari kwamba mitambo ya Tume ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo halisi kufanyiwa ukarabati.

IEBC imekuwa ikitangaza matokeo ya awali ya urais mtandaoni, na kwa sasa matokeo hayo yalikuwa yanamuonyesha Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee akiwa mbele na kura 7,795,083 (54.38%) naye Bw Odinga akiwa na kura 6,433,161 (44.76%).

Matokeo hayo ni ya kutoka vituo

38561 kati ya vituo 40883 nchini humo.

Kura zilizoharibika kufikia sasa ni 382,705

Bw Odinga, akiandamana na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, na viongozi wengine wakuu wa muungano huo, amesema wadukuzi walitumia taarifa alizokuwa nazo meneja wa teknolojia wa IEBC Chris Msando aliyeuawa wiki moja iliyopita kuingia katika mitambo ya IEBC.

Waziri huyo mkuu wa zamani amesema baada ya kuingia, wadukuzi walitumia programu fulani kuongeza matokeo ya Rais Kenyatta na kupunguza matokeo yake.

Amesema anaamini hilo lilifanyika katika kaunti zote na kwamba wagombea wa NASA katika nyadhifa nyingine waliathirika pia.

Bw Odinga, amesema huo ulikuwa "ulaghai wa hali ya juu".

Hata hivyo, ametoa wito kwa wafuasi wa muungano huo waendelee kuwa watulivu.

Bw Musyoka amesema anawashauri wafuasi wa muungano huo waendelee na shughuli zao za kawaida, ingawa huenda karibuni wakatakiwa kuchukua hatua.

Bw Odinga na Kalonzo wamekataa kusema ni hatua gani zaidi watachukua na badala yake wakasema wanasubiri kusikia ufafanuzi kutoka kwa IEBC kuhusu yaliyotokea.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amewaambia wanahabari baadaye kwamba wamepata habari kuhusu tuhuma za muungano huo wa upinzani kwamba mitambo yao ya uchaguzi ilidukuliwa.

Amesema tume haiwezi kupuuza tuhuma kama hizo na kwamba maafisa wake watafanya uchunguzi kubaini iwapo kuna ukweli wowote katika madai hayo.

Hata hivyo alieleza imani yake kwamba mfumo wa uchaguzi unaotumiwa na tume hiyo ni imara na kwamba ulitumiwa na shughuli zote za awali, na sasa "imesalia shughuli ya mwisho" ya kupeperusha na kutangaza matokeo ya kura.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527