MADIWANI WATATU WA CHADEMA WAJIUZULU NA KUTIMKIA CCM HAI KILIMANJARO

Wakati Wimbi la Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujiunga na Chama cha Mpinduzi (CCM) likiwa limepamba moto mkoani Arusha, majirani zao wa Kilimanjaro nao wameanza kutimka kwa kile wanachodai kuwa ni kumuunga mkono Rais Dkt John Pombe Magufuli.


Mapema leo mchana Julai 26, 2017, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewapokea madiwani watatu kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai ambao wametangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kujiunga CCM.


Madiwani waliojiuzulu ni, Diwani wa Kata ya Machame Magharibi, Goodluck Kimaro, Diwani wa Kata ya Weruweru, na Diwani wa Kata ya Mnadani, Everist Peter Kimati.


Akizungumza wakati wa kutangaza azma hiyo, Goodluck Kimaro alisema kwamba CHADEMA hakuna demokrasia kama ambavyo chama hicho kimekuwa kikijinasibu. 


Akitolea mfano Halimashauri ya Wilaya ya Hai ambapo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe ni Mbunge wa jimbo hilo, alisema chama hakina uwezo wa kufanya jambo lolote dhidi ya mbunge.


Endapo mbunge atashindwa kutekeleza majukumu yake, chama ndio kinatakiwa kumuadhibu, lakini kwa upande wetu wa Hai hakuna uongozi wa kuweza kufanya hivyo. 


Mbunge huwa hafanyi ziara za kutembelea jimbo kama anavyotakiwa, lakini bado chama hakina sauti, alisema Goodluck Kimaro.


Baada ya madiwani wote kuzungumza, Polepole alionya juu ya uwepo wa vitendo vya kihalifu kwa madiwani ambao wanahama CHADEMA na kusema jambo lolote likitokea kwa madiwani hao waliohama, watashughulikiwa ipasavyo na vyombo vya dola lakini pia chama hicho kingine ndio watakuwa wahusika.


Hadi sasa jumla ya madiwani 9 mkoani Arusha tayari wamejiunga na CCM na sasa watatu mkoani Kilimanjaro nao wamejiunga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527