MGEJA: WAKUU WA MIKOA,WILAYA MSIOGOPE KUTUMBULIWA,SEMENI UKWELI KUHUSU BAA LA NJAA


WAKUU wa mikoa na wakuu wa wilaya nchini wametakiwa kujitokeza hadharani kutoa tamko rasmi la baa la njaa linalowakabili wananchi kwenye maeneo yao wanayoyaongoza.

Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation Khamis Mgeja alisema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari alipokuwa anatoa salamu za mwaka mpya akiwa mkoani Tabora kwa mapumziko ya sikukuu ya mwaka mpya 2017.

Mgeja alisema anawaomba kwa heshima wasiogope kusema ukweli kwa woga wa kutumbuliwa na mamlaka za juu zilizowateua kwani hali ya baa la njaa nchini ni kubwa katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini.

Alisema inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wakikaa kimya na ukimya huo unawaumiza wananchi huku viongozi hao wakifumbia macho jambo hili eti kwa hofu ya kutumbuliwa.

Alisema ni lazima wakuu wa mikoa na wa wilaya watambue cheo ni dhamana na hakuna mtu aliyezaliwa na uongozi bali watambue uongozi ni matokeo tu yanayomkuta mwanadamu katika mchakato wa maisha yake.

Aidha alisema uongozi siyo jambo la kudumu na  na nje ya ukuu wa mkoa na wilaya  kuna maisha hivyo kutokana na baa la njaa lililopo kwenye baadhi ya maeneo, wakuu wa wilaya na mikoa wakubali kuwa kafara na kujitoa sadaka kwa ajili ya wananchi kwa kujitokeza kusema ukweli.

Mgeja alisema tatizo lililopo la njaa kwenye baadhi ya maeneo
linapelekea baadhi ya wananchi kulalia uji na wengine maembe na hili ni janga kubwa kwa taifa.

Alisema hakuna aibu wala kosa kusema ukweli lakini tatizo lililopo la nchi yetu umezuka ugonjwa mbaya sana wa uoga na hofu kwa viongozi na watendaji baadhi kwa sasa wana hofu na uoga wa kiutendaji wakihofia kutumbuliwa.

Mgeja alisema faida ya kusema ukweli itasaidia serikali kujipanga vizuri hivyo kuiomba serikali pia iwe sikivu kwa suala la njaa linalokabili wananchi na kwamba ni lazima viongozi wawe wanawapa wananchi maneno ya matumaini kuliko kuwakatisha tamaa.

Alisema serikali kuwaaeleza wananchi kuwa ‘serikali haina shamba wala chakula cha bure’ au ‘mwafaa’ maneno hayo hayaleti afya wala matumaini kwa wananchi wanaowaongoza.

Alimshauri waziri mkuu Kassim Majaliwa kwamba kuanzia sasa katika ziara zake anapotembelea miradi mbalimbali katika wilaya na mikoa hasa iliyokumbwa na baa la njaa basi atembelee na shehena ya chakula cha njaa.

Mgeja alimuomba Waziri Mkuu pia awe anatanguliza chakula cha njaa sehemu anazokwenda kwani kitengo cha maafa kiko chini yake na wapo wananchi wanaohitaji chakula cha bure na wapo wanaohitaji kuhudumiwa.

Alisema wapo pia wanaojiweza lakini uwezo wao ni mdogo wa kumudu bei za sokoni zilizopo sasa na kama chakula cha serikali kikiwafikia bei yake itakuwa chini na watu kipato cha chini watamudu kununua chakula hicho.

Mgeja aliiomba na kuishauri serikali kulipa kipaumbele suala hilo na hasa katika kilimo cha mwaka huu mazao yameanza kunyauka kutokana na ukame mkubwa kutokana na  mvua kutonyesha vya kutosha.

Aliishauri na kuiomba serikali ya awamu ya tano iweke wazi juu ya akiba ya chakula kuwa kuna kiasi gani ili wananchi wajue kwani ni haki yao kwa sababu chakula ni cha umma na wana haki kujua.

"Serikali inaposhindwa kusema ukweli kuhusu baa la njaa eti kwa sababu ya kiusalama wa kitaifa sasa tunajiuliza je chakula nacho kimekuwa zana za ‘Kivita’?, ni vyema serikali ikawa wazi kuhusiana na akiba ya chakula ili wananchi wapate fursa ya kujipanga vizuri kwa kujifunga mkanda",aliongeza Mgeja.

Na Hastin Liumba-Malunde1 blog Tabora

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527