MAPYA YAIBUKA SAKATA LA ASKOFU MOKIWA KUTUMBULIWA DAR


KATIBU Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Johnson Chinyong’ole amesema aliyekuwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentine Mokiwa anakabiliwa na mashitaka ya jinai kwa kuingia mikatiba mibovu na matumizi mabaya ya fedha za kanisa makosa yanayoangukia kuvunja sheria za nchi.

“Hatujakurupuka kuchukua hatua, ushahidi wote tumeshauwasilisha kwa vyombo vinavyohusika serikalini, sisi tumetimiza wajibu wetu, hivyo tunaviachia vyombo vinavyohusika kufanya kazi yake katika eneo hilo la ubadhirifu wa fedha,” alisema Chinyong’ole.

Alifafanua kuwa wakati wanaenda kutangaza uamuzi wa kumvua uaskofu Dk Mokiwa juzi kanisa la Ilala, walienda kutoa taarifa kwa msajili wa vyama ambaye ndiye anayesajili makanisa, lakini pia wameshatoa taarifa katika ofisi za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria.

Alitaja sheria alizovunja Dk Mokiwa kuwa ni sheria ya miunganiko ya wadhamini sura ya 318, sheria ya ardhi namba 4 ya 1999 na sheria ya mipango miji sura ya 355 kwa kuruhusu mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika shamba la kanisa la Mtoni Buza na eneo la Kanisa la Mtakatifu Mariam Kurasini.

“Sisi tunasubiri mrejesho kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Rita na kwa Msajili wa vyama vya kiraia,” alisema katibu mkuu huyo wa kanisa la Anglikana Tanzania.

Alifafanua kuwa katika mashitaka 10 anayokabiliwa nayo, shitaka la tatu ndilo ambalo ni la ubadhirifu wa mali za kanisa ndilo ambalo linaifanya serikali kuingilia kati.

Alisema makosa ya Dk Mokiwa yanahusisha pia kughushi na akatoa mfano wa kuingia mikataba kwa kuwatumia watu ambao si wadhamini wa kanisa hilo wakati sheria inamtaka atumie wadhamini wawili wanaosimamia mali za kanisa, pamoja na kutumika kwa muhuri bandia wakati sheria inasisitiza muhuri unaotumika ni ule wa moto.

Katibu Mkuu huyo alisema ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma dhidi ya askofu hiyo yenye kurasaa 173 imewasilishwa pia serikalini ili vyombo vinavyohusika kufuatilia tuhuma hizo viweze kujiridhisha wakati vinapoenda kuchukua hatua.

“Hakuna mtua aliyeonewa, wala kuchafuliwa, hizi ni tuhuma za ubadhirifu wa mali ya kanisa, lazima vyombo vya dola vihusike hapa,” alisema katibu mkuu huyo na kuongeza kuwa serikali ndio inayotakiwa kuchukua hatua kwa sababu tume iliyoundwa na kanisa imeshaweka hadharani ushahidi kwa lengo la kuokoa mali za kanisa.

Amevunja kiapo cha utii Kwa hali hiyo jambo hilo tayari wameliwasilisha kwa msajili wa vyama ambaye ndiye msajili wa kanisa hilo na pia wamewasilisha suala hilo kwa wakala wa vizazi na vifo (Rita) kwa kuwa sheria ya nchi iliyovunjwa ni ya udhamini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Chinyong’ole alisema kwa mujibu wa katiba ya kanisa hiyo ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, pamoja na Dk Mokiwa kugoma kung’oka madarakani baada ya kuvuliwa madaraka yake na askofu mkuu Dk Jacob Chimeledya, kwa sasa katiba haimtambui kama askofu wa kanisa hilo.

Alisema kabla ya marekebisho ya mwaka 2004, sinodi ya dayosisi ndio ilikuwa inakuwa na tamko la mwisho dhidi ya askofu wa dayosisi, lakini baada ya marekebisho kufanyika askofu mkuu ndiye msimamizi wa maaskofu wote wa dayosisi na ana mamlaka ya kuwastaafisha pale wanapokiuka katiba ya kanisa.

“Dk Mokiwa amenyang’anywa utawala wa dayosisi ya Dar es Salaam, katiba inampa mamlaka askofu mkuu kuwastaafisha maaskofu ikibainika wameenda kinyume cha sheria na katiba ya kanisa,” alisema Chinyong’ole.

Aliongeza kuwa baada ya kumvua utawala wa dayosisi, hatua inayofuata ni taratibu zingine za kisheria ambazo zitashughulikiwa na kanisa ikiwa ni pamoja na kumbana Dk Mokiwa kukiuka kiapo chake cha kumtii askofu mkuu wa kanisa.

Alisisitiza kuwa Dk Mokiwa amevunja kifungu namba 7 cha katiba ya kanisa hilo kuhusu kiapo cha utii kwa askofu mkuu aliposema

“Nakubali na kuahidi kumheshimu na kumtii, kama inipasavyo, askofu mkuu wa kanisa Anglikana Tanzania... watakaofuata baada yake...”

Katibu mkuu huyo alisema Dk Mokiwa kutokana na hatua yake kugoma kujiuzulu baada ya kushauriwa na askofu mkuu Tanzania, amevunja kiapo cha utii kwa katiba ya jimbo kinachosema,

“Ninaahidi pia kwamba nitakubali kujiuzulu au kujitoa kwa hukumu yoyote itakaoniachisha madaraka na mapato yanayohusika na dayosisi hii nitakayohukumiwa wakati wowote baada ya uchunguzi wa kutosha wa barza lenye kbali cha sinodi ya kanisa.”

Pia amevunja kiapo cha utii kwa katiba ya dayosisi kinachosema “Ninaahidi pia kwamba nijiuzulu wakati wowote kama ikiazimiwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania kwa mujibu wa katiba ya kanisa na ya Dayosisi.”

Wachunguzi wa mambo wanabainisha kuwa kugoma kwa Dk Mokiwa kung’oka madarakani kutaleta mtafaruku mkubwa ndani kanisa hilo kutokana na baadhi ya makanisa katika Dayosisi ya Dar es Salaam kuunga mkono uamuzi wa askofu mkuu na wengine wanamuunga mkono Dk Mokiwa.

Juzi, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Jacob Chimeledya alimvua uaskofu mkuu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Mokiwa baada ya mashitaka 10 yaliyofunguliwa na walei 32 wa kanisa hilo katika dayosisi hiyo kumtuhumu kwa ufisadi wa mali za kanisa hilo.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu kama ilivyoshauri nyumba ya maaskofu ambayo ilimkuta na hatia ya ufujaji wa mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kiuchungaji ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi ya kanis ahilo nchini.

Hata hivyo, Dk Mokiwa amegomea uamuzi huo kwa maelezo kuwa, mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Salaam ambayo ndio yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si askofu mkuu au askofu mwingine yeyote wa kanisa la Anglikana Tanzania.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527